Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kongamano la kwanza la awali la kielimu kwa mnasaba wa milenia ya Hawza ya kielimu ya Najaf Ashraf, lenye anuani isemayo “Urithi wa kielimu wa Sheikh Tusi katika upeo wa fikra za Kiislamu na Magharibi; tafakuri na mitazamo ya kisasa”, litafanyika kwa uenyeji wa Haram Tukufu ya Hadhrat Abbas (a.s.).
Tukio hili la kielimu, lenye kaulimbiu “Hawza ya Najaf Ashraf… miaka elfu ya kujitolea na kufanya khidma” na likiwa na mhimili wa “Urithi wa Sheikh Tusi katika fikra za Kiislamu na Magharibi; mitazamo ya kisasa”, litafanyika tarehe 11 na 12 Februari 2026 (22 na 23 Bahman 1404) mjini Najaf Ashraf.
Kwa mujibu wa waandaaji, kongamano hili ni sehemu ya mkusanyiko wa programu pana za kufufua urithi wa kielimu wa Hawza ya Najaf, na linalenga kusoma upya nafasi ya kihistoria na ya ustaarabu ya Sheikh Tusi katika muundo wa fikra za Kiislamu pamoja na kufafanua athari zake katika tafiti za kisasa ndani ya ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi.
Katika kongamano hili, wasomi miongoni mwa watafiti na maprofesa wa Hawza na vyuo vikuu watawasilisha makala za kitaaluma, wakichambua mafanikio ya kielimu ya Sheikh Tusi na kutathmini nafasi yake katika maendeleo ya elimu za fiqhi, usuli, kalamu na tafiti linganishi.
Waandaaji walisisitiza kuwa tukio hili ni mwanzo wa mfululizo wa programu za kielimu na kitamaduni zilizoandaliwa kwa miaka ijayo kwa mnasaba wa milenia ya Hawza ya kielimu ya Najaf Ashraf.

Maoni yako